Je Nyota Zina Mapigo?
Juni 12, 2013

Picha hii inaonyesha maelfu ya nyota ambazo ukiziangalia kwa mbali zinaonekana kufanana: Kama nukta za miale ya mwanga zenye kupendeza. Lakini ukiziangalia kwa karibu zinaonyesha aina tofauti tofauti ya rangi, ukubwa na jotoridi: kutoka katika nyota baridi nyekundu na ndogo hadi zile zenye kung’aa sana za blu na kubwa! Na wakati ambapo nyingi ya nyota hizi zinatumia muda wake mwingi kuunguza haidrojeni katika viini vyake na kumeremeta, zingine zipo active zaidi ya hapo. Aina mpya ya nyota iliyogunduliwa inafanana kabisa na aina ya pili ya nyota!

Aina hii ya nyota ni “pulsating variable” na imepewa jina hili kwa sababu kung’aa kwake kunabadilika kwa kadri zinavyozidi kutanuka na kusinyaa kama moyo unavyodunda. Kubadilika kwa mng’ao wa nyota hizi ni kutoka katika mng’ao mkubwa hadi mdogo; unaoweza kudumu kwa sekunde chache au miaka kutokana na aina ya nyota inayobadilika. Nyota hizi hutanuka na kusinyaa kutokana na hali maalum na nguvu kubwa inayofanya kazi ndani yake.Hivyo basi kwa kuziangalia nyota hizi tunaweza kujua siri ya ni nini kinachotokea ndani yake. Taarifa ambazo zisingeweza kupatikana kwa njia nyingine

Kwa muda wa miaka saba wanaastronomia wamekuwa wakizisoma nyota 2000 za blu na nyekundu kutoka katika kundi lililopo kati kati ya picha hii. Wamegundua kuwa nyota 36 zinafuata mfumo tofauti na usiotarajiwa. Zimekuwa zikionyesha mabadiliko madogo lakini yanayojirudia rudia katika mng’ao wake. Kama moyo unaodunda kila baada ya masaa mawili mpaka ishirini. Kitu kama hiki hakikutarajiwa kabisa na mpaka sasa hakuna anayeweza kusema ni kwanini nyota hizi zinabadilika katika mtindo huu. Tuna dokezo moja tu, kuwa nyota hizi zinazunguka haraka kulinganisha na nyota nyingine zinazofanana nazo. Tunatarajia kuwa wataalamu watagundua ni kwanini nyota hizi zina tabia hii inayofanana na kudunda kwa moyo muda si mrefu!

Dokezo

Ulijua kuwa Jua letu ni aina ya nyota zinazobadilika badilika? Nishati inayotolewa na Jua inabadilika kila baada ya miaka 11! Na mabadiliko haya madogo yanaweza kuiathiri Dunia kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano kati ya mwaka 1645 na 1715 Jua lilipita kipindi cha kutoa nishati ndogo. Wakati huo huo bara la Ulaya lilipatwa na baridi kali sana: Mto Thames uliopo London uliganda, barafu ilitapakaa katika milima ya Alps na barafu katika bahari ya Kaskazini iliongezeka!

 

This Space Scoop is based on a Press Release from ESO .
ESO

Mponda Malozo / UNAWE-Tanzania

Picha
Chapisha

Bado una shauku? Jifunze zaidi...

Space Scoop ni nini?

Vumbua astronomia zaidi

Hamasisha kikazi kipya cha wavumbua anga

Marafiki wa Space Scoop

Wasiliana nasi